Vifungu vya 24 na 25 vya Sheria Nambari 3 ya BMEJZ inatoa
mamlaka kwa Bodi kukusanya na kusimamia marejesho yote ya mikopo kwa wanafunzi
wa elimu ya juu waliosoma kwa mkopo kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Kila mdaiwa ni lazima alipe deni lote
analodaiwa na Bodi likijumuisha fedha alizolipwa mkononi na zilizolipwa moja
kwa moja kupitia akaunti za huo alichosoma. Mkopo utaanza kurejeshwa mara tu
baada ya mkopaji kuhitimu masomo yake na kuajiriwa katika taasisi za umma au
sekta binafsi au kujiajiri mwenyewe. Mkopaji anaweza kurejesha mkopo wake wote
kwa pamoja au kwa makataa ndani ya muda maalum uliowekwa na Bodi kulingana na
kima cha mkopo aliopewa.
·
Kutoa taarifa kwa uongozi wa BMEJZ kuhusu
kuhitimu masomo yake na kupata ajira.
·
Kutoa taarifa sahihi ziwemo anwani ya makazi,
mwajiri au pahala pa kazi endapo mkopaji atakuwa ni mjasiriamali.
·
Kuanza marejesho ya mkopo kwa kumtaka mwajiri
wake kukata deni analodaiwa na BMEJZ kutoka katika mshahara wake wa kila mwezi
na kuwasilisha mikato hiyo ofisi za Bodi kwa utaratibu ambao Bodi itaona
unafaa.
· Mdaiwa aliyejiajiri anaweza kuanza marejesho ya mkopo kwa hiari kwa kadiri ya kiwango anachoweza baada ya makubaliano maalum na BMEJZ.
Adhabu kwa Wanaokwepa Kurejesha Mikopo yao
Endapo mkopaji atashindwa kurejesha
mkopo baada ya kufika kwa muda wa marejesho,
·
Atalazimika kulipa kiasi chote cha mkopo na
gharama nyenginezo zinazoweza kutokea kutokana na kukwepa kulipa mkopo wake
ikiwa pamoja na tozo ya mawakili.
·
Bodi inaweza kumfikisha kwenye vyombo vya
sheria na kufungua mashtaka ya madai kwa mkopaji atakayekiuka wajibu wake wa
kulipa deni analodaiwa na Bodi.
·
Kutozwa faini isiyopungua shilingi 50,000 kwa
mwezi kwa kila marejesho ambayo
hayatowasilishwa kwa wakati stahiki
· Bodi inaweza kuchukua hatua nyengine zozote, kwa mujibu wa sheria, itakazoona zinafaa dhidi ya mdaiwa.
·
Mkopaji ambaye wakati wa kuomba mkopo hakuwa
na ajira, anapaswa kuanza marejesho yake baada ya kumalizika kipindi cha mwaka
mmoja cha msamaha (grace period) tokea kuhitimu masomo yake.
·
Mkopaji ambaye wakati wa kuomba mkopo alikuwa
ni mwajiriwa au amejiajiri, anapaswa kuanza marejesho ya mkopo mara tu baada ya
kuhitimu masomo yake au ndani ya muda wowote ambao Bodi itaona unafaa.
· Mkopaji anapaswa kuendeleza mfululizo wa marejesho ya mkopo wake ndani ya muda uliowekwa na BMEJZ bila ya kusita kwa marejesho hata kwa mwezi mmoja. Hata hivyo Bodi inaweza kubadilisha muda wa mwisho wa marejesho kulingana na kiwango cha deni, uwezo wa kulipa wa mkopaji, utayari na uaminifu wa mkopaji kulipa deni lake, muda wa mkataba wa ajira uliobaki kabla ya kustaafu
Rufaa kwa Wasiriodhika na Madeni
yao
Mkopaji ambaye hatoridhika na deni lake
atakalokabidhiwa na Bodi baada ya kuhitimu masomo yake anaweza kukata rufaa kwa
kuomba kufanyika uhakiki mpya ya deni lake kwa utaratibu ambao Bodi itaona
unafaa. Muombaji mwenye haki ya kukata rufaa na kusikilizwa ni yule ambaye:
a) Ametoa
taarifa kwa Bodi mara baada ya kuhitimu masomo yake.
b) Amewasilisha
rufaa yake ndani ya siku 30 tokea tarehe aliyopokea barua ya kumjulisha deni
lake na inayomtaka kuanza taratibu stahiki za kuanza marejesho ya mkopo wake.
c) Amewasilisha
barua ya rufaa pamoja na nyaraka zote muhimu na zilizothibitishwa na mahakama
au wakili zikiwemo transcript na
cheti cha kuhitimu masomo; kivuli cha kitambulisho cha Mzanzibari; risiti ya
malipo ya gharama za rufaa;
d) Barua
yake ya rufaa inaonesha vipengele anavyodai vipitiwe upya na Bodi.
e) Ameanza
kurejesha deni lake wakati anasubiri kutolewa maamuzi ya rufaa yake.