Loan

MCHAKATO WA UTOAJI WA MIKOPO

Mikopo hutolewa kwa waombaji wa elimu ya juu waliotimiza sifa na vigezo kama vinavyoainishwa na kifungu cha 20 cha Sheria Namba 3/2011 na kifungu cha 3 cha Kanuni za Bodi.

Kulingana na tafsiri iliyotolewa na Sheria ya Bodi, elimu ya juu ni ngazi ya elimu inayoanzia Shahada ya Kwanza (Bachelor/First Degree) au ngazi nyengine ya mafunzo inayolingana na shahada ya kwanza na kuendelea.

Elimu ya juu hutolewa na vyuo vikuu na vyuo vyengine vya elimu ya juu ndani na nje ya nchi vinavyotambuliwa na mamlaka husika nchini zikiwemo Kamisheni ya Vyuo Vikuu (Tanzania Commission for Universities – TCU) na Baraza la Mafunzo ya Ufundi (The National Council for Technical Education - NACTE).

Mamlaka ya Utoaji Mikopo ya BMEJZ

Sheria Namba 3 ya 2011 inatoa mamlaka kwa BMEJZ ya kuongoza na kusimamia mchakato wa utoaji mikopo kwa waombaji kulingana na mahitaji na uwezo uliopo kwa wakati husika. Mamlaka ya Utoaji Mikopo ya BMEJZ ni pamoja na:

a)   Kuamua vipengele vya mafao ya  mkopo atakavyopatiwa muombaji;

b)   Kuweka vigezo na sifa za msingi kwa muombaji wa mkopo;

c)   Kuweka masharti maalum ya utoaji wa mikopo;

d)   Kuamua idadi ya waombaji watakaopata mkopo kwa kila mwaka; na

e)   Kusimamia fani za masomo kulingana na vipaumbele vya SMZ wakati wa utoaji wa mikopo.

Kifungu cha 19(1) cha Sheria ya Bodi kinaitaka BMEJZ kutoa mkopo kwa kila muombaji, aliyetimiza vigezo na sifa za msingi za kupatiwa mkopo zilizowekwa na BMEJZ, ili aweze kulipa gharama zote au sehemu ya gharama za elimu ya juu kwa kipindi chote atachokuwa masomoni. 

Uteuzi wa Waombaji Watakaopatiwa Mikopo

Taarifa zilizoingizwa kwenye mfumo wa kompyuta hutumika kutoa mapendekezo ya awali ya uteuzi wa waombaji wa mikopo ambao wametimiza sifa za msingi za uteuzi kwa mwaka husika.  Orodha ya waombaji kwa kila ngazi ya masomo inayoombwa kulingana na uzito wa sifa za kila muombaji na fani iliyoombwa hutayarishwa kwa ajili ya uteuzi.

Vigezo vinavyotumika kutoa mapendekezo ya awali ya uteuzi wa waombaji watakaopatiwa mikopo unafuata utaratibu uliowekwa na vifungu vya 19 na 20 vya Sheria Namba 3/2011 ya BMEJZ na kufafanuliwa na vifungu vya 3 hadi 5 vya Kanuni za BMEJZ. Kwa ujumla vigezo vinavyotumika kutoa mapendekezo ya uteuzi ni kama vifuatavyo:

·       Alama za ufaulu za waombaji.

·       Kuwepo kwa ithibati ya mwanafunzi kukubaliwa kujiunga na chuo husika kabla ya uteuzi.

·       Fani inayoombwa kulingana na vipaumbele vya SMZ.

·       Umri wa muombaji.

·       Uwiano wa idadi ya waombaji katika fani mbalimbali.

·       Uwiano wa idadi ya waombaji wanaume na wanawake wanaopendekezwa kupatiwa mikopo.

·       Uwezo wa fedha wa BMEJZ kutoa mikopo kwa waombaji katika mwaka husika.

·       Uwepo wa waombaji waliopatiwa mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ya Jamhuri ya Muungano au Taasisi na Asasi nyengine zinazotoa udhamini wa masomo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.

Kwa mujibu wa kifungu cha 12 cha Sheria Namba 3/2011 na kifungu cha 8 cha Kanuni za BMEJZ, mapendekezo ya uteuzi wa majina ya waombaji wa mikopo yanatakiwa kuwasilishwa kwenye Kamati ya Elimu ya Juu inayoundwa na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa BMEJZ. Kazi ya Kamati ya Elimu ya Juu ni kuhakiki, kujadili na kupitisha majina ya waombaji walioteuliwa kupatiwa mikopo katika mwaka husika kwa kuzingatia vigezo vilivyotajwa hapo juu au vyenginevyo kwa kadiri Kamati ya Elimu ya Juu itakavyoona inafaa kwa wakati husika.

Hata hivyo, Kamati ya Elimu ya Juu imekasimu madaraka yake kwa Kamati ya Uteuzi ambayo uwepo wake umetimiza matakwa ya kisheria kama ilivyotajwa katika kifungu cha 14(5) cha Sheria ya BMEJZ. Kamati ya Uteuzi inaundwa na wajumbe watano wasiokuwa Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya BMEJZ. Wajumbe wa Kamati ya Uteuzi wanateuliwa na Mhe. Waziri anayesimamia shughuli za Elimu.

Wajumbe hao watatoka:

·       Tume ya Mipango ya SMZ.

·       Wizara inayosimamia Elimu.

·       Wizara inayosimamia Utumishi wa Umma.

·       Sekta binafsi.

·       Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (BMEJZ), ambayo itawakilishwa na Meneja Mikopo atakayekuwa pia Katibu wa Kamati ya Uteuzi.

Baada ya kumaliza kazi ya uteuzi wa waombaji wa mikopo ya elimu ya juu, Mwenyekiti ya kamati ya Uteuzi atakabidhi taarifa ya uteuzi’ pamoja na orodha za majina ya waombaji wanaopendekezwa kupatiwa mikopo, kwa mwenyekiti wa Kamati ya Elimu ya Juu ambaye ataiwakilisha katika Kikao cha Bodi ya Wakurugenzi wa BMEJZ kwa ajili ya kuridhiwa na kutoa idhini ya kutangazwa kwa waombaji wote waliopatiwa mikopo.

Majina ya waombaji walioteuliwa kupatiwa mikopo hutangazwa kupitia tovuti ya BMEJZ (www.zhelb.go.tz), tovuti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo wa Amali (www.moez.go.tz) au njia nyengine yoyote ambayo BMEJZ itaona inafaa na inayoweza kuwafikia watu wengi zaidi kwa urahisi.


  Idadi ya Waombaji Wanaoteuliwa Kupatiwa Mikopo

Hakuna idadi maalum iliyowekwa ya waombaji wanaoteuliwa kupatiwa mikopo kwa mwaka husika katika ngazi mbalimbali za masomo. Idadi ya wanaoteuliwa inategemea upatikanaji wa fedha za kutosha kukidhi mahitaji ya idadi kubwa ya waombaji wapya wa mikopo na idadi ya wanafunzi wanaoendelea na masomo yao vyuoni kupitia mikopo wanayopatiwa na BMEJZ.

Wakati wa uteuzi kipaumbele hutolewa kwa waombaji wanaotoka kwenye familia zenye kipato kidogo; wanawake na walemavu au wazazi wa muombaji wote ni walemavu au wenye maradhi ya kudumu na kuthibitishwa na daktari anayetambulika kuhusiana na kutokumudu kwao kujiingizia kipato cha kuweza kumlipia gharama za masomo mtoto wao.

Hivyo waombaji wenye uwezo wa kujilipia gharama za masomo au wanaotoka kwenye familia zenye uwezo wa kulipa gharama za masomo wanashauriwa kutokuomba mikopo kutoka BMEJZ ili kutoa nafasi kwa waombaji wasiojiweza kutumia nafasi chache za mikopo zilizopo.

  Sifa za Kupata Mkopo

Sifa za waombaji wa mikopo ambao maombi yao yanaweza kuzingatiwa wakati wa uteuzi zimetajwa kwenye kifungu cha 20 zikiwemo:

a)   Muombaji awe Mzanzibari

b)  Awe ameomba mkopo kwa kujaza Fomu Nambari 1 au kupitia njia nyengine yoyote ile ambayo BMEJZ itaona inafaa. Maombi yawe yamewasilishwa ndani ya muda maalum uliowekwa na BMEJZ unaoanzia Mei 2 hadi Julai 31 ya kila mwaka.

c)   Awe amepata udahili kwenye chuo cha elimu ya juu kinachotambuliwa na mamlaka husika nchini.

d)   Awe amepata alama nzuri za ufaulu.

         i.        Muombaji wa shahada ya kwanza (Bachelor/First Degree) aliyehitimu kidato cha sita anapaswa awe amefaulu angalau masomo mawili ya mlinganisho (Principal subjects) kwa alama za ufaulu zinazoanzia alama (points) 4.0.

         ii.    Muombaji wa shahada ya kwanza aliyehitimu stashahada ya kawaida (Ordinary Diploma) anatakiwa awe na ufaulu unaoanzia alama (GPA) 3.0 au B. Wahitimu wa “Full Technician Certificate (FTC)” wawe na ufaulu unaoanzia alama C.

        iii.    Muombaji wa shahada ya uzamili (Master/Second Degree) katika masomo ya sanaa au sayansi jamii awe amehitimu shahada ya kwanza na kupata alama za ufaulu kuanzia daraja la pili la juu (upper second class). Waombaji wa shahada ya uzamili katika masomo ya sayansi, ufundi, tiba, uchumi, mipango na biashara wawe na alama za ufaulu za kuanzia daraja la pili la chini (lower second class). Wahitimu wa stashahada ya uzamili(Postgraduate Diploma) wanapaswa kupata alama za ufaulu kuanzia daraja la pili la chini (lower second class)

       iv.    Muombaji wa shahada ya uzamivu (Doctor of Philosophy - PhD) awe amehitimu shahada ya uzamili na kupata alama za kuanzia daraja la pili la juu kwa waombaji wa masomo ya sanaa na sayansi jamii. Waombaji wa shahada ya uzamivu katika masomo ya sayansi, ufundi, udaktari na uchumi, mipango na takwimu wapate alama za ufaulu kuanzia daraja la pili la chini.

         v.    Waombaji wanaoendelea na masomo vyuoni pia wanaweza kuomba kwa kuzingatia sifa za kitaaluma zilizotajwa hapo juu [d(i) –(iv)]. Aidha muombaji awe amefaulu mitihani yake ya chuo kwa kiwango kitakachomwezesha kuendelea na masomo kwa mwaka unaofuatia katika ngazi ya masomo anayoombea mkopo.

Angalizo: Bodi inaweza kupitia upya sifa za kitaaluma kwa waombaji wa mikopo kulingana na mahitaji ya wakati husika.

 

e)     Awe ameomba fani inayolingana na vipaumbele vya SMZ katika mwaka husika.

f)      Asiwe na mkopo au udhamini wa masomo kutoka taasisi nyengine.

g)    Muombaji wa shahada ya kwanza asizidi umri wa miaka 35 wakati wa kuanza masomo na muombaji wa shahada ya uzamili asizidi miaka 40. Ukomo wa umri wa muombaji wa shahada ya uzamivu ni miaka 45 wakati wa kuanza masomo.

h)    Muombaji aliyeajiriwa kwenye utumishi wa umma awasilishe barua ya ruhusa kutoka kwa mwajiri wake.

i)      Muombaji anayedaiwa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar awe ameshaanza kulipa deni lake kwa angalau asilimia 25 ya deni lote bila ya kusita kwa malipo ya deni ya kila mwezi.

j)      Muombaji aliyesoma kwa mkopo kutoka BMEJZ awe ameshafanya kazi kwa angalau miaka miwili baada ya kuhitimu masomo yake ya awali kabla ya kuomba mkopo mwengine kutoka BMEJZ.

Angalizo:

·       Waombaji wanaotumia sifa za masomo ya kidato cha nne kuomba udahili katika vyuo vikuu vya ndani au nje ya nchi ili kujiunga na masomo ya Shahada ya Kwanza, maombi yao ya mkopo hayatozingatiwa. Mfumo wa elimu wa Tanzania unaotumika kwa wakati huu unatambua sifa ya msingi kwa wahitimu wa elimu ya sekondari wanaodahiliwa kwa masomo ya Shahada ya Kwanza au ngazi inayolingana nayo katika vyuo vikuu na vyuo vyengine vya elimu ya juu ni kuhitimu masomo ya kidato cha sita.

Vilevile, waombaji wa mikopo waliohitimu masomo ya Diploma pasi na kuwa na elimu ya kidato cha sita au sifa za kujiunga na kidato cha sita, wanatakiwa wawe wamefaulu angalau masomo matano ya kidato cha nne kwa kiwango cha alama D na kuhitimu ngazi ya cheti (Certificate) kabla ya kujiunga na masomo ya Diploma (NTA 6).

 Fani za Vipaumbele wa Kipindi cha Miaka Mitano 2016 - 2020

Tume ya Mipango ya SMZ imetoa taarifa kuhusu utafiti uliofanywa juu ya hali ya utumishi nchini ambayo imeonesha uwepo wa mahitaji makubwa ya wataalamu. Taarifa hiyo imeibua maeneo ya Vipaumbele vya SMZ juu ya mahitaji ya wataalamu na imeagizwa kuwa taarifa hiyo itumike kama kigezo muhimu kwa utoaji wa mafunzo ya elimu ya juu nchini ili kufikia utekelezaji wa mipango na maendeleo ya rasilimali watu iliyo bora na itakayowaandaa watu wenye ujuzi sahihi, taaluma, tabia na silka zenye tija zinazoendana na mabadiliko ya mfumo wa ushindani wa soko la ajira na kufikia viwango vya juu vya uzalishaji na utoaji huduma.

Ili kurahisisha utekelezaji wa Vipaumbele vya SMZ katika utoaji wa mafunzo ya elimu ya juu kuanzia mwaka wa masomo 2016/17 hadi 2019/20, Tume ya Mipango imevigawa vipaumbele hivyo katika madaraja matatu tofauti kulingana na umuhimu wa kila kada kama inavyoonekana katika jedwali la hapo chini.

Hivyo, kwa mwaka huu wa masomo, BMEJZ itazingatia kikamilifu taarifa ya fani za vipaumbele ya Tume ya Mipango wakati wa upokeaji wa maombi ya mikopo na uteuzi wa waombaji katika mwaka wa masomo 2017/18.

SEKTA

FANI NA KIWANGO CHA KIPAUMBELE

DARAJA LA KWANZA

DARAJA LA PILI

DARAJA LA TATU

EDUCATION

Science and Mathematics

Curriculum Development

Learning Materials Development

 

Technical Vocational Training

School science Laboratory Management

 

 

Early Primary Education

IT with Education in Science Subjects/Mathematics

 

 

Geography and English language

 

 

 

Geography and History

 

 

 

History and English

 

 

HEALTH

Anaesthesiology

Cardiology

Biochemistry

 

Dentistry

Dermatology

Chemistry

 

Gastroenterology

Endocrinology

ENT

 

Haematology

General Surgeon

General Medicine

 

Medical imaging

Medical Emergency

Infectious diseases

 

Neurosurgery

Oncology

Microbiology

 

Obstetrics and Gynaecology

Paediatric surgery

Nephrology

 

Opthalmology

Physiotherapy

Pharmacology

 

Orthopaedic

Psychiatry

Pharmacy

 

Pathology

Neurology

Plastic surgery

 

Radiology

Nursing and Midwifery

Rheumatology, Allergy and Immunology

 

Urology

 

Virology

LAND AND ENERGY

Cartography

Architect

Environment Health Surveying

 

Land Management

Mining/Metallurgy Engineering

 

 

Land Surveying

Quantity Surveying

 

 

Urban Planning

Radiation Protection

 

 

 

Renewable Energy and Atomic Energy

 

PETROLEUM AND GAS

Geology

 

Petroleum Law

 

Petroleum Chemistry

 

 

 

Petroleum Engineering

 

 

 

Geophysics

 

 

 

Petroleum Economics

 

 

 

Environmental Engineering (Oil and Gas)

 

 

INDUSTRIES

Biological/Chemical Laboratories Technicians

 

 

 

Chemical Engineering

 

 

 

Industrial Engineering (Production, Quality Assurance, Product Design)

 

 

 

Soil Expertise

 

 

 

Water Engineering

 

 

 

Water management

 

 

TRADE

Trade Economics

International Business

Trade Administration

TOURISM

Tourism Marketing

Language Professions

 

 

Cultural heritage and Conservation

Tourism Management

 

 

Hospitality

 

 

 

Tourism Planning

 

 

AGRICULTURE

Aquaculture

Agro Forests

Agriculture Planning

 

Irrigation Engineering

Animal breading

Agronomy

 

Plant Breeding

Animal Nutrition

Animal Husbandry

 

Plant Pathology

Biotechnology

Fisheries Science

 

Soil science Disciplines

Entomology

Marine Science

 

 

Food and nutrition

Seed Technology

 

 

Horticulture

 

 

 

Microbiology

 

 

 

Natural resources management

 

 

 

Veterinary

 

FINANCE

Financial Market and Investment

Insurance

Banking and Business Administration

 

Financial Management

Procurement

Tax Management

 

Programme Analysis

Risk and  Damage Evaluation

 

TRANSPORT AND COMMUNICATION

Computer Science and Engineering

Port and Shipping Management

 

 

Information, Communication Technology (ICT)

Road Economists

 

 

Telecommunication Engineering

Pilot and Aircraft Engineering

 

ENVIRONMENT

Natural Resources Management

Environment Impact Assessment

 

 

 

Environment Planning and Management

 

 

 

Waste Management

 

ECONOMICS AND DEVELOPMENT PLANNING

Monitoring and Evaluation

Building Economics

 

 

Specialized Economics (Educational health, development etc).

Entrepreneurship

 

 

Statistics

Human Resource Management, Planning and Development

 

 

 

International Development Policy and Negotiation

 

 

 

Local Government

 

OTHER PROFESSIONAL

 

 

Mass Communication

 

 

 

International Relations

 

 Mafao ya Mikopo

Mafao ya mkopo ambayo BMEJZ inaweza kutoa kwa muombaji yameanishiwa kwenye Kifungu cha 19(2) cha Sheria Namba 3/2011. BMEJZ inaweza kutoa kwa ukamilifu au sehemu ya mafao ya mkopo yaliyoainishwa ambayo yanajumuisha:

a)   Ada ya masomo

b)   Ada ya mitihani

c)   Posho la chakula na makazi

d)   Gharama za vitabu na vifaa vyenginevyo vya kujifunzia

e)   Nauli (inayoweza kulipwa ama mwanzo na mwisho wa kila mwaka wa masomo kwa wanafunzi wa vyuo vya ndani; au kulipwa mwanzo wakati muombaji anakwenda chuoni kuanza masomo na baada ya kuhitimu masomo ya mwaka husika kwa vyuo vya nje.)

f)    Posho la utafiti na/au kazi za vitendo

g)   Gharama kwa ajili ya mahitaji maalum ya vitivo

h)  Bima ya afya

Hata hivyo, Bodi imepewa mamlaka ya kisheria ya kuamua vipengele vya mafao ya mkopo atakavyopatiwa mwanafunzi husika na vipengele vitavyobakia vichangiwe na mwanafunzi mwenyewe, mzazi au mlezi wa mwanafunzi husika.

Masharti ya Mikopo

a)   Kila muombaji atakayeteuliwa kupata mkopo awe tayari kujaza mkataba wa mkopo (Fomu Nambari 2) unaotolewa na BMEJZ na kukamilisha taarifa zote pamoja na kufuata masharti yote yaliyoainishwa kwenye mkataba. Mkataba huu unapaswa kujazwa mwanzo wa mwaka wa masomo kwa wanafunzi wapya na kurejea kujaza mkataba mpya kila mwanzo wa mwaka mpya wa masomo kwa wanafunzi wanaoendelea na masomo kwenye ngazi ya masomo waliyokubaliwa kupatiwa mkopo na BMEJZ.

b)   Malipo ya ada ya masomo, ada ya mitihani na gharama nyengine zinazopaswa kulipwa moja kwa moja kwa chuo zitalipwa kupitia akaunti ya chuo husika au njia nyengine ambayo BMEJZ itaona inafaa. Mtiririko wa malipo ya ada ya masomo utalingana na muda wa masomo wa ngazi husika kama utakavyoelezwa kwenye barua ya udahili.

c)   Posho zinazopaswa kulipwa moja kwa moja kwa mwanafunzi, BMEJZ italipa kupitia akaunti itakayofunguliwa na mwanafunzi kwa maelekezo ya BMEJZ au njia nyengine ambayo BMEJZ itakayoona inafaa. Malipo ya posho yatalipwa kulingana na vigezo na uwezo wa Bodi. Kwa wanafunzi wa vyuo vya nje, malipo ya posho yatafanyika kulingana na kiwango cha ubadilishaji fedha za kigeni kilichotumika wakati wa kupitishwa kwa bajeti.

d)   Malipo ya mkopo yatatolewa kwa utaratibu wa awamu au mkupuo kulingana na mfumo wa masomo katika Chuo husika au BMEJZ itakavyoona inafaa kulingana na uwezo wake.

e)   Kiwango cha mkopo utakaotolewa kitakuwa na ukomo wa mwisho wa malipo (ceiling) wa gharama za masomo kwenye ngazi husika katika mwaka husika wa masomo. Mwanafunzi husika atawajibika kujilipia gharama za ziada. Ukomo wa mwisho  wa malipo kwa mwaka wa masomo kwa wakopaji wa shahada ya kwanza ni shilingi 6,000,000/=; wakopaji wa shahada za uzamili shilingi 8,000,000/= na shahada za uzamivu ni shilingi 10,000,000/=.

f)    Wakopaji waliodahiliwa kwenye fani zinazosomeshwa na vyuo vya ndani ya nchi kwa kushirikiana na vyuo vya nje ya nchi ambapo ada ya masomo hutozwa kwa shilingi ya Tanzania kwa ajili ya chuo cha ndani na fedha za kigeni kwa ajili ya chuo cha nje na kulipwa katika akaunti tofauti, BMEJZ italipa ada inayotozwa kwa shilingi za Kitanzania pekee. Sehemu ya ada inayotozwa kwa fedha za kigeni italipwa na mwanafunzi husika.

g)   Wakopaji waliojiunga/wanaojiunga na vyuo vya nje kusoma fani adimu na zilizo kwenye vipaumbele vya SMZ watapatiwa aina moja ya mafao ya mkopo kulingana na chaguo lake au kwa njia yoyote ile ambayo BMEJZ itaona inafaa. Utaratibu huu umewekwa ili kuiwezesha BMEJZ kutoa mikopo inayorejesheka na kuongeza idadi ya waombaji wanaopatiwa mikopo.

h)  Muombaji atakayerejea mwaka wa masomo katika ngazi husika, atapatiwa ruhusa ya kuendelea kupatiwa mkopo kwa mwaka mmoja wa ziada kulingana na muda wa masomo wa ngazi husika.

i)    Muombaji ataruhusiwa kuahirisha masomo na kurejea masomoni mwaka unaofuata mara moja tu katika muda wote wa masomo katika ngazi ya masomo anayopatiwa mkopo. Mkopaji atakayeshindwa kurejea masomoni mwaka unaofuata baada ya kuahirisha, mkopo wake utasitishwa na kutakiwa kuanza marejesho ya mkopo.

j)    Muombaji aliyeajiriwa asiwe na madeni kutoka taasisi nyengine yanayofikia zaidi ya theluthi moja ya mshahara wake kabla na hadi atakapomaliza mkataba wake wa mkopo na Bodi.