Students

 Wajibuwa wa Mwanafunzi Mkopaji

Kila mkopaji atakuwa na wajibu wa kutekeleza yafuatayo:

1.     Kujaza mkataba wa mkopo unaotolewa na BMEJZ kila mwaka husika wa masomo, kukamilisha taarifa zote anazopaswa kuzitoa na kutekeleza masharti ya mkataba kikamilifu.

2.     Kuwa na wadhamini wasiopungua wawili watakaokubali kwa maandishi kulipa mkopo huo kwa BMEJZ kwa niaba ya mkopaji endapo kwa sababu yoyote ile mkopaji atashindwa kulipa mkopo wake.

3.     Kuijulisha BMEJZ kuhusu mabadiliko yoyote yale yanayoweza kuathiri utoaji wa mkopo kwa namna yoyote ile, kama vile, kuacha chuo, kushindwa kuendelea na masomo chuoni kwa sababu yoyote ile. Endapo mwanafunzi husika hatotoa taarifa na BMEJZ ikaendelea na kufanya malipo kwa mwanafunzi huyo, malipo hayo yatajumuishwa kwenye deni lake na atalazimika kulilipa lote.

4.       Kuwasilisha ankara ya malipo (invoice) kutoka chuo husika mapema iwezekanavyo ili BMEJZ iweze kufanya malipo kwa wakati unaofaa. Hakuna mwanafunzi atakayefanyiwa malipo ya ada bila ya kuwasilisha Ankara ya malipo inayoonesha mchanganuo wa gharama kwa kila kifungu cha malipo.

5.       Ankara ya malipo itakayowasilishwa ijumuishe taarifa kamili zitakazoiwezesha BMEJZ kufanya malipo kwa usahihi zikiwemo

a)     Jina la akaunti ya Chuo (Account/Payee/Beneficiary’s name);

b)    Nambari ya akaunti ya chuo (Account/Payee/Beneficiary’s account)

c)     Jina la benki inayotumiwa na chuo (Bank Name)

d)    Alama ya Utambalisho wa malipo (Swift Code)

6.       Kudai risiti ya malipo kila baada ya BMEJZ kufanya malipo na kuiwasilisha BMEJZ kwa masawazisho.

7.       Kuweka saini kwenye fomu maalum za malipo  zitakazotolewa na BMEJZ ili kuthibitisha kiwango cha malipo kilicholipwa kwa ajili yake na kuwasilishwa BMEJZ. Fomu hiyo lazima iwe imeshawekwa saini na kuwasilishwa ofisi za BMEJZ ndani ya siku thelathini (30) tokea tarehe ya kuwasilishwa fomu hiyo Chuoni.

8.     Endapo mkopaji atakwepa kuweka saini kwenye fomu maalum, BMEJZ inaweza kusitisha mkopo wake na kiwango cha malipo kilicholipwa kinaweza kuhamishiwa kwa mkopaji mwengine au kikabaki na kuwa sehemu ya deni lake analopaswa kulilipa mara moja.

9.     Kuwasilisha matokeo yake ya mwisho wa muhula/mwaka kwa BMEJZ kabla ya kuendelea kulipiwa mkopo kwa awamu nyengine. Muombaji ambaye hatowasilisha matokeo yake kwa wakati, BMEJZ inaweza kusitisha malipo kwa muhula/mwaka mpya.

10.  Kutoa taarifa kwa BMEJZ endapo ataamua kufanya malipo yoyote chuoni, ikiwemo ada, ambayo kwa mujibu wa mkataba BMEJZ ndiyo inayopaswa kufanya malipo hayo. Taarifa hiyo itolewe kabla BMEJZ kufanya malipo stahiki chuoni hapo. Endapo itagundulika kuwa mkopaji amefanya malipo chuoni bila ya kutoa taarifa au kupata idhini ya BMEJZ:

a)   Mkopaji aliyefanya malipo hayo hatokuwa na haki ya kuomba kurejeshewa fedha hizo na BMEJZ. Marejesho yoyote ya fedha yaombwe kutoka chuo husika.

b)   BMEJZ itasita kumlipia mkopaji malipo ya ada ya masomo na mitihani na gharama nyenginezo.

c)   Malipo yote yaliyofanywa na BMEJZ yatajumuishwa kwenye deni la mkopaji pasi na kujali malipo aliyoyafanya mwenyewe kabla na baada ya kupata udhamini wa BMEJZ.

11.  Kuipatia BMEJZ taarifa nyengine zozote zile zinazohusiana na mkopo wake pale atakapotakiwa kufanya hivyo.

12.  Kuwasilisha taarifa kamili za akaunti yake binafsi ya benki itakayoweza kutumiwa na BMEJZ kufanya malipo ya posho la kujikimu na stahiki nyenginezo kwa ajili ya mkopaji kila itakapowezekana.

Uhamisho wa Mkopo

Ili kuwawekea wanafunzi mazingira mazuri ya kujifunza, BMEJZ inaruhusu mwanafunzi kuhamisha mkopo kutoka chuo kimoja hadi kingine baada ya kutimiza masharti yafuatayo:

·       Kutoa taarifa ya maandishi kwa BMEJZ juu ya dhamira yake ya kuhamisha mkopo na kueleza sababu za msingi zitakazoweza kuushawishi uongozi wa BMEJZ kuridhia uhamisho huo. Taarifa hiyo itolewe kwa utaratibu ambao BMEJZ itaona unafaa.

·       Kuambatanisha nyaraka zinazohalalisha uhamisho wake zikiwemo barua kutoka chuo cha awali kinachomkubalia kuhama; barua ya kukubaliwa kujiunga na chuo kipya anachohamia kuendelea na masomo.

·       Uhamisho ufanyike ndani ya siku 14 tokea siku ya kwanza ya kutangazwa kwa majina ya waombaji wapya walioteuliwa kupatiwa mkopo.

·       Fani atakayosoma kwenye chuo kipya iwe miogoni mwa Vipaumbele vya SMZ.

·       Mwaka wa masomo unaoombewa uhamisho kutoka chuo cha awali uwe sawa na mwaka wa masomo ambao muombaji ataendela na masomo katika chuo kipya. Uhamisho hautatolewa kwa mwanafunzi aliyeshindwa kuendelea na masomo katika mwaka husika.

·       Kuwasilisha risiti inayothibitisha kufanyika kwa malipo ya gharama za kushughulikia mchakato wa uhamisho. Kiwango cha malipo kitaamuliwa na uongozi wa BMEJZ kulingana na wakati husika.

·       Mwanafunzi aliyeshindwa kuendelea na masomo hataruhusiwa kuhamisha mkopo kwenda chuo kingine.

Usitishaji wa Mkopo

Bodi ya Wakurugenzi ya BMEJZ inaweza kusitisha mkopo likitokea mojawapo kati ya yafuatayo:

1.     Mkopaji kufukuzwa chuo kutokana na utovu wa nidhamu au kujishughulisha na vitendo vya jinai

2.     Mkopaji kutoendelea na masomo kutokana na kutofaulu mitihani ya muhula au/na mwisho wa mwaka.

3.     Mkopaji kutoa taarifa za udanganyifu kwa kudhamiria au vyenginevyo. Mwanafunzi husika atatakiwa kurejesha kiasi chote cha mkopo alichokopeshwa.

4.     Mkopaji kuacha chuo/kuahirisha masomo bila ya sababu zozote za msingi zinazokubaliwa na BMEJZ ama kwa kutoa taarifa au bila ya kutoa taarifa kwa BMEJZ. Mwanafunzi husika atatakiwa kurejesha kiasi chote cha mkopo alichokopeshwa.

5.     Mkopaji kurejea masomo (repeating) zaidi ya mara moja.

6.     Mkopaji kupata mkopo kamili, sehemu ya mkopo au udhamini wa masomo kutoa taasisi nyengine. Mwanafunzi husika atawajibika kurejesha mara moja mkopo wote aliokopeshwa na BMEJZ.

7.     Mkopaji kwa hiari yake kuiomba Bodi kusitisha mkopo anaopatiwa.

8.     Mkopaji kuhama chuo kimoja na kuhamia chuo kingine bila ya kutoa taarifa kwa BMEJZ au kutowasilisha vielelezo vinavyomkubalia kuhama chuo cha awali na kuhamia chuo kipya vikiwemo barua ya ruhusa ya kuhama chuo, matokeo ya mtihani kutoka chuo anachohama na barua ya kujiunga na chuo kipya.

9.     Mkopaji kubadilisha fani bila ya kutoa taarifa na kuridhiwa na BMEJZ au kuchagua fani isiyo katika Vipaumbele vya SMZ.

10.  Kutojaza mkataba mpya na BMEJZ kwa kutoa au kutokutoa taarifa kwa BMEJZ.

11.  Kutotia saini kwenye fomu maalum za uthibitisho wa malipo (Fomu Nambari 3) zinazotolewa na BMEJZ.

12.  Kujitokeza kwa kitendo chochote kile ambacho uongozi wa BMEJZ utaridhia kuwa ni sababu toshelevu ya kusitisha mkopo.